Kuna wakati maisha tunayoishi, yanatufanya tusahau kuna mwisho,
Si kwamba hatujui ila ni ngumu kuifikiri hiyo siku.
Hususani pale amani, vicheko furaha na raha tele, zinapokuwa ni sehemu ya haya maisha.
Na hata changamoto zitujiapo ndani
Tunajipa moyo kuwa bado tuna muda wa pamoja kuweza kutatua
Pasipo kujua mmoja wetu atatwaliwa mapema hivi
Chorus
Eee Mungu tunaomba utukumbukeee wakati huu,
Tumeondokewa na mpendwa wetu Raymond,
Jana alikuwa sawa tu, tulipanga mengi kama siku nyingine
Ila leo kazima kama mshumaa upulizwapo na upepo,
Mke wako anakulilia mbona umelala mapema,
Watoto wako wanakutafuta baba umeenda wapi
Ona wazazi, ndugu na marafiki,wanalia hawana la kufanya
Ooooh yote ni ya Mungu hatuna budi kushukuru.
Neno lako Yesu linasema
Upo karibu nao waliovunjika mioyo, na unawaokoa waliopondeka roho." Naomba usituache,
Maana msaada wa karibu ni wewe Yesu,
Hata katika hili ni wewe Baba
Nyakati za uchungu nakutegemea wewe kimbilio letu na msaada pia unaoonekana wakati wa taabu na shida na uchungu
Chorus
Eee Mungu tunaomba utukumbukeee wakati huu,
Tumeondokewa na mpendwa wetu Raymond,
Jana alikuwa sawa tu, tulipanga mengi kama siku nyingine
Ila leo kazima kama mshumaa upulizwapo na upepo,
Mke wako anakulilia,
Watoto wako wanakutafuta
Ona wazazi, ndugu na marafiki,
Ooooh yote ni ya Mungu.
(Maombi)
*Baba yetu uliye mbinguni,*
Tunakuja mbele zako tukiwa na huzuni kubwa kwa sababu ya kuondokewa na mpendwa wetu. Wewe ndiye Mungu wa faraja zote na Baba wa rehema. Leo tunamweka mbele zako mke wa marehemu pamoja na watoto wake.
Bwana, wakumbatie kwa upendo wako. Pale ambapo mioyo yao imevunjika, uwe mponyaji wao. Pale ambapo machozi yanatiririka, uwape faraja ya Roho Mtakatifu. Wape nguvu ya kustahimili siku hizi ngumu na uwape tumaini linalotokana na wewe.
Tunakuomba uwalinde na kuwahifadhi. Uwaondolee hofu ya kesho na uwape amani inayopita ufahamu wa kibinadamu. Wakumbushe kwamba wewe ni Baba wa yatima na mtetezi wa wajane, na kwamba hutawaacha wala kuwatelekeza.
Bwana, wape hekima katika maamuzi yatakayofuata, uwazungushe na watu wenye upendo na moyo wa kuwasaidia, na uimarishe familia yote ili ibaki katika umoja na upendo.
Tunawaombea na ndugu wote wa marehemu. Wape nguvu, uvumilivu, na neema ya kupitia kipindi hiki kwa kukutegemea wewe.
Tunaweka tumaini letu kwako, tukijua kwamba hata katikati ya majonzi, wewe bado ni mwaminifu na upo pamoja na watu wako.
Katika jina la Yesu Kristo, tunaomba na kuamini. Amina.